Mali za Marehumu Kanumba Zagawanywa Hivi
HUKU sakata la mirathi ya marehemu Steven Charles Kanumba aliyekuwa gwiji wa filamu Bongo, likiendelea kufukuta chini kwa chini, baba mzazi mzee Charles Kusekwa Kanumba amegawanya mali za mwanaye, Risasi Mchanganyiko linakufunulia.Mali za marehemu Kanumba zinazotajwa katika mgawo huo ni pamoja na kampuni yake iitwayo Kanumba The Great Film Company na magari.
HABARI KAMILI
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Shinyanga, mzee Kusekwa (pichani) alisema yeye kama baba wa marehemu ana jukumu la kuwa msimamizi wa mirathi na kugawa mali za mwanaye.
“Tumekaa huku Shinyanga na ndugu wengine, hili suala la mirathi linapaswa kuwa chini yangu kwa sababu mimi ndiye baba. Kimila za kikwetu (Kisukuma), msimamizi wa mirathi huwa ni baba,” alisema mzee Kusekwa.
Akaongoza: “Kutokana na hilo, nimechukua jukumu la kugawa mali za marehemu mwanangu kwa kuzingatia usawa, haki na vigezo muhimu.”
MGAWANYO WENYEWE
Katika mgawo huo, mzee Kusekwa alitaja sehemu za mali za marehemu Kanumba huku akiacha nyingine.
Mali ambazo hakuzitaja na zinajulikana ni pamoja na akaunti za benki, viwanja viwili vilivyopo Mbezi, Msakuzi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na mali nyingine.
Aliwataja mama mzazi wa marehemu, Flora Mtegoa, mdogo wa Kanumba aliyekuwa akifanya naye kazi kwa karibu enzi za uhai wake, Seth Bosco.
Alisema, katika mgawo huo yeye kama baba anastahili kuchukua gari la kifahari alilokuwa akitumia mwanaye wakati wa uhai wake, aina ya Toyota Lexus na Bi. Mtegoa achukue gari ndogo aina ya Toyota GX 110.
“Ile kampuni ya filamu (Kanumba The Great Film Company) watachukua Seth na dada yake,” alisema mzee Kusekwa.
Kwa sasa, wanaosimamia kampuni hiyo iliyopo Sinza, Mori, jirani na Baa ya Meeda jijini Dar es Salaam ni Seth na dada yake aitwaye Bela.
MPANGO WAKWAMA
Wakati hayo yakiendelea, ilielezwa kuwa mzazi huyo alituma wawakilishi wake kutoka Shinyanga hadi jijini Dar kwa lengo la kufungua mirathi.
Habari za ndani kutoka kwa chanzo chetu makini ambacho hakikupenda jina litajwe gazetini, zinasema kwamba wawakilishi hao walifika katika Mahakama ya Mwanzo ya Kinondoni lakini walikwama.
“Hawafanikiwa kufungua mirathi maana hawakuwa na vielelezo vya kutosha. Walitakiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa na cha kifo cha Kanumba pamoja na vielelezo vingine ambavyo hawakuwa navyo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Basi baada ya kukwama, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kurudi Shinyanga.”
MAMA KANUMBA
Mama wa marehemu Kanumba, Bi. Mtegoa alipoulizwa anachofahamu kuhusu ujio wa wawakilishi wa mzazi mwenzake alisema: “Nilisikia wamekuja, lakini sijapata kuwaona kabisa. Tumesubiri mpaka sasa kuona kama tutaitwa mahakamani lakini hatujaitwa.”
Akaongeza: “Kiukweli sijui nini kimetokea, maana siku chache baada ya arobaini ya mwanangu, tuliweka kikao hapa Dar na mwenzangu (baba Kanumba) alituma watu wawili waliokuja kumuwakilisha.
“Baada ya makubaliano hayo, tuliwekeana sahihi wanandugu wa pande zote mbili na hata baba Kanumba alikubaliana na watoto wake waliokuja kumuwakilisha kuhusu uteuzi huo...sasa haya tena yananishangaza maana hata mahakamani kufungua mirathi bado sijaenda.”