|

Kocha mpya Yanga mambo safi


Clara Alphonce na Jessca Nangawe
MABINGWA  wa Kombe la Kagame, Yanga ya jijini Dar es Salaam, watamtangaza kocha wao mpya Ijumaa wiki hii, ambapo ataanza kazi rasmi mara baada ya michuano ya Kombe la Kagame baadaye mwezi ujao.
Kwa maana hiyo, Kocha Msaidizi, Fred Minziro ndiye atakayeketi kwenye benchi na kuiongoza timu hiyo inayovaa jezi za rangi ya njano na kijani kutetea taji hilo.
Awali, Yanga ilibainisha kuwa inasaka kocha mwenye uzoefu na soka la Afrika pamoja na mazingira yake kama ilivyokuwa kwa kocha aliyeondoka, Kostadin Papic raia wa Serbia.
Kiongozi wa usajili wa Yanga, Seif Ahmed alithibitisha kuwa kocha toka Ubelgiji, Tom Saintfiet ni miongoni mwa wawili wenye nafasi kubwa kutua Jangwani.
Na kwa upande wa Katibu wa Yanga, Selestine Mwesigwa ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo kwa sasa, alisema kuwa majina ya makocha watatu yameshapitishwa.
"Kulikuwa na maombi ya makocha 25, baada ya mchujo tumechagua makocha watatu ambao tunawachuja na kumtangaza mmoja wiki hii," alisema.
Alisema timu inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Kaunda tayari kwa maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame itakayoanza Julai 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakati huohuo, Kelvin Yondani aliyejiunga Yanga toka Simba, amesema katika kipindi kifupi alichofanya mazoezi klabu yake hiyo mpya, amebaini kuwa hakufanya makosa kutua Jangwani.
Yondani alisema kuwa, maisha ya Jangwani ni mazuri hasa ukizingatia kuwa amepata mapokezi na ushirikiano mzuri na wachezaji na viongozi.
Pia ametumia fursa hiyo kuitaka Simba kumsahau kwani yeye tayari ni mali ya Yanga na hakuna jitihada zozote za kujaribu kumrudhisha Simba zitakazofanikiwa.
Uhamisho wa Yondani ulizua utata mkubwa baada ya klabu yake ya zamani kudai ni mchezaji wao halali, huku Yanga na mchezaji wenyewe wakisema tofauti.
"Sifahamu kwanini Simba bado wanazungumza mambo haya. Mimi nimeshamaliza kila kitu na Yanga, ni vizuri wakaniacha nifanye kazi Yanga," alisema Yondani.

Posted by Unknown on 11:13 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added