Bilioni 300 za vigogo Uswisi zatikisa nchi
KUBAINIKA kwa Sh303.7 bilioni zilizofichwa katika akaunti za vigogo wa Serikali na wanasiasa nchini Uswisi, kumetikisa nchi huku shinikizo likitolewa kwa vyombo vya dola kuchunguza haraka na kuchukua hatua za kisheria, ikiwamo kurejesha fedha hizo.
Jana kutwa nzima, gazeti hili lilipokea simu kadhaa kutoka kwa wasomaji wake wakiwamo wabunge na mawaziri, huku baadhi wakichangia maoni kwenye tovuti na mtandao mbalimbali ya kijamii, wakitaka kujua majina ya wamiliki wa akaunti hizo.
Bungeni mjini Dodoma, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliitaka Serikali kuchunguza tuhuma hizo kisha kuwachukulia hatua watu sita wanaotajwa kwamba wanamiliki akaunti zenye mabilioni hayo ya shilingi chini Uswisi.
Fedha hizo zimebainishwa na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB), iliyotolewa hivi karibuni, ikitaja nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, na kiwango cha fedha zilizohifadhiwa huko.
Tayari Kitengo cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kimeeleza kuwapo kwa fedha hizo katika benki mbalimbali nchini Uswisi, zilizoingizwa na kampuni za uchimbaji mafuta na madini.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nayo imeweka bayana kuwa inafuatilia suala hilo kwa mamlaka za Uswisi, ili kujua fedha hizo ziliko na nani anazimiliki.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine ambazo zina fedha nyingi katika benki za Uswisi ni Kenya (dola 857 milioni), Uganda (dola 159 milioni), Rwanda (dola 29.7 milioni) na Burundi dola 16.7 milioni.
Chanzo cha habari hizo, kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe, wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi moja.
Kauli ya Zitto
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aliliambia Bunge jana kuwa haiwezekani nchi ikaendelea ilhali watu wanakusanya fedha kutokana na utafiti wa gesi na mafuta, ambao bado haujaanza kulinufaisha Taifa.
Akichangia Bajeti ya Waziri Mkuu, Zitto alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) ielekezwe ili ifanye uchunguzi utakaowezesha wamiliki wa akaunti hizo kufahamika, ili wachukuliwe hatua mara moja bila kujali nafasi wanazozishikilia ndani ya Serikali.
“Viongozi wanaohamisha na kupeleka fedha za Watanzania nje ya nchi wanatakiwa wachukuliwe hatua mara moja. Hili litatusadia katika siku zijazo, kwani kama wapo wengine wanaodhani wanaweza kuficha fedha zao nje basi wajue kwamba popote watakapozipeleka tutazifuata na kuzirejesha,” alisema Zitto na kuongeza;
“Namuomba Waziri Mkuu aagize uchunguzi ufanyike, fedha hizi zirejeshwe na wahusika wachukuliwe hatua,” alisema Zitto.
Zitto alitoa kauli hiyo akiyanukuu magazeti ya Mwananchi, The Citizen na The East African ambayo kwa nyakati tofauti yameandika kuhusu kuwapo kwa kiasi kikubwa cha fedha zinazotokana na rushwa, ambazo zimehifadhiwa kwenye akaunti kadhaa nchini Uswisi.
Alisema kuachia suala hilo kuendelea ni hatari, kwani uchumi wa nchi utahujumiwa hata kabla ya miradi husika haijaanza kutekelezwa.
“Haiwezekani sisi tupo tunahangaika kutafuta gesi na mafuta huko baharini Lindi na Mtwara, halafu watu wengine tayari wameishawekewa hela kwenye akaunti, kwa hakika lazima uchunguzi ufanyike na watu hawa wajue kwamba Serikali ina uwezo wa kuwafahamu na kurejesha hizo fedha hizo nchini,” alisema Zitto.
Alitoa mfano wa Serikali ya India ambayo iliwahi kupata taarifa za baadhi ya watumishi wake kuficha fedha nchini Uswisi na kuchukua hatua za kiuchunguzi zilizowezesha wahusika kutajwa hadharani, kisha fedha zilizoibwa serikalini kurejeshwa.
Katika hatua nyingine, Zitto alitaka mvutano baina ya Tanzania Bara na Visiwani kuhusu masuala ya gesi umalizwe ili kuwezesha utafiti kuendelea kufanywa katika maeneo ya bahari ya Hindi.
Alisema utafiti katika baadhi ya maeneo hasa eneo la Bahari karibu na kisiwa cha Pemba umesimama kutokana na mvutano wa iwapo suala la mafuta ni la Muungano au la.
“Kama visiwani watavumbua gesi ni sawa, wavumbue kivyao, na sisi Tanzania bara tumeshavumbua matrilioni ya gesi, basi tuendelee kivyetu lakini tusisimamishe tafiti kutokana na mvutano usio na maslahi kwa nchi,” alisema.
Lowassa atoa kauli
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge Edward Lowassa, alisema jana kuwa kamati yake imesikia suala hilo kwenye vyombo vya habari na inajipanga kuzifanyia kazi taarifa hizo mara moja.
"Tumesikia kupitia vyombo vya habari na kama kamati tutahakikisha tunazifanyia kazi," alisema Lowassa alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano aliouitisha kuzungumzia safari ya kamati yake nje ya nchi.
Chadema yatoa tamko
Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeonya kuwa tatizo la ufisadi halitaisha nchini hadi pale Serikali itakapochukua hatua za dhati za kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote ambao wamehusika na ufisadi wa raslimali za nchi.
Chama hicho kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuagiza kukamatwa kwa watuhumiwa wote wa ufisadi wa ununuzi wa rada na wale ambao wanatuhumiwa kuhifadhi Sh 303.7 bilioni nchini Uswisi.
“Chadema kinatambua kwamba kuachwa kwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua kamili za kisheria na mali zao kufilisiwa, kunafanya taifa kuendelea na ufisadi ikiwemo ule wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Richmond na sasa tuhuma mpya za ufisadi wa shilingi bilioni 303 kwenye akaunti Uswisi,” ilisema Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, kupitia taarifa kwa
vyombo vya habari jana.
Wizi mwingie kupitia mtandao
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Pereira Ame Silima alilieleza Bunge jana kuwa hadi sasa kiasi kilichoripotiwa Polisi kuhusina na wizi kwa njia ya mtandao nchini ni Sh2.2 bilioni.
Fedha hizo ni zimegawanywa katika makundi matatu, Sh1.3 bilioni, Euro 8,897 (Sh17,660, 545) na dola 551,777 (Sh882,843,200).
Kauli hiyo ilitolewa wakati Waziri Silima akijibu swali la Hussein Mussa Mzee (Jang’ombe-CCM) aliyetaka kujua ni kiasi gani cha fedha kimeripotiwa Polisi kutokana na wizi kwa njia ya mtandao.
Mzee alihoji Serikali imejipanga vipi kudhibiti wizi wa mtandao, idadi ya waharifu wa wizi huo ambao wamekamatwa huku akitaka itungwe sheria maalumu kushughulikia wizi huo.
Silima alisema kuwa Serikali imetunga sheria inayoshughulikia uhalifu unaofanywa kwa njia ya mtandao, Electronic and Posta Communication Act, 2010 na sheria ya kudhibiti fedha haramu (The Anti – Money Laundering Act – 2006.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia vyombo mbalimbali vya dola kama vile Polisi, taasisi za fedha, vyombo vya habari, TRA na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imejiwekea mikakati ya kuelimisha wananchi kuhusu aina ya uharifu wa kimtandao na jinsi ya kupambana nao.
Waziri alibainisha kuwa jeshi la Polisi limeanzisha Kitengo cha Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Unit) ambacho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kinafanya kazi kubwa ya kupambana na majanga hayo.
Kilio cha wabunge
Wakati huohuo wabunge wameendelea kumbana Pinda huku baadhi yao wakikataa kuunga mkono hotuba yake hadi pale atakapojibu hoja walizotoa.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy akichangia hotuba ya hiyo jana, alisema vita dhidi ya ufisadi haiwezi kufanikiwa kwani vyombo vya husika wakiwamo Takukuru wanashindwa kuchukua hatua kwa makosa ambayo yako wazi.
Keissy alisema mafisadi na walarushwa nchini wanalindwa na Takukuru, kwani licha ya kuwapo kwa ushahidi na viashiria vya wazi, chombo hicho hakichukui hatua zozote.
Alisema, kama wapo watu wanaodiriki kuuza dawa ambazo zilipaswa kupelekwa katika hospitali na matokeo yake wagonjwa wanakufa, mtu huyo hana budi kunyongwa.
“Sheria za nchi hii zinawalinda wezi, ndiyo maana ufisadi hauwezi kuisha, mtu ana majengo makubwa leo, wakati ni jana tu amepata ubunge, amepata wapi utajiri huo wa haraka, aulizwe na akishindwa kutoa maelezo achukuliwe hatua,” alisema Keissy na kuongeza:
“Sasa la ajabu ni kwamba eti wanakwambia kwamba kama unamjua mla rushwa basi uwapelekee taarifa, kwani wao hawawaoni watu wanaotajirika haraka haraka?” alihoji.
Keissy ambaye aliipinga Bajeti ya Waziri Mkuu hadi pale atakapopewa majibu ya kuridhisha, alisema sheria za nchi hii ni dhaifu, ndiyo maana mafisadi wanaoiba mamilioni wanaendelea kudunda barabarani wakati mwizi anayeiba simu hupigwa na kuchomwa moto hadi kufa.
Mbunge huyo alisisitiza ujumbe wake, akisema kuwa, “hata ikitokea mafisadi hao wakafariki basi pingu ziwekwe juu ya makaburini yao.”
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Riziki Lulida alisema kuna njama zinazofanyika za kudhoofisha maendeleo mkoani Lindi kwa kuwapeleka viongozi wala rushwa katika mkoa huo.
Alisema, uduni wa mkoa huo unasababisha wapinzani kuufanya kuwa kichaka cha wapinzani, kuwadhalilisha na kuwasema kwamba wao ni maskini.
“Viongozi wengi wa halmashauri wanaofanya ubadhirifu wa fedha kutoka mikoa mingine hutupwa Lindi,” alisema Lulida kabla ya kuanza kuwataja kwa majina wafanyakazi hao wa halmashauri:
“Joachim Materu ameiba 577 milioni, akapelekwa Lindi, Eunice Maro ameiba 262 milioni na akapelekwa Lindi, baada ya kufanya wizi huo, Maro aliziweka katika akaunti inayoshukiwa kuwa ni ya rafiki yake, yenye akaunti namba 206660017 NMB ambaye alihamishiwa Ofisi ya Kilimo Lindi,” alisema.
Aliwataja wengine kuwa ni Macha anayetuhumiwa kuiba Sh6 bilioni ambaye amehamishiwa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na kwamba kuhamishwa kwao ni kusambaza ufisadi katika maeneo mengine.
Lulida aliongeza kuwa, kama Waziri Mkuu anataka aiunge mkono bajeti yake, basi aje na majibu sahihi kuhusu maendeleo mkoani Lindi pamoja na kurudisha programu ya kilimo ya Kanda ya Kusini, (SAGCOT)
Habari hii imeandaliwa na Neville Meena, Florence Majani na Habel Chidawali, Dodoma na Leone Bahati Dar