|

Fredy Minziro bado adai chake Yanga


WAKATI kocha wa Yanga, Fredy Minziro akikazia kauli yake ya awali kutowafundisha mabingwa hao wa Kombe la Kagame mpaka atakapolipwa malimbikizo ya mishahara yake, mchezaji Shamte Ally naye ameugomea uongozi wa klabu hiyo unaodaiwa kutaka kumtoa kwa mkopo kwenda Toto African ya Mwanza.

Shamte, nyota wa zamani wa Kagera Sugar amesema hayuko tayari kwenda kuicheza Toto msimu ujao na badala yake atabaki mpaka mkataba wake utakapofikia kikomo katikati ya mwaka ujao.Mbali na Minziro kuweka msimamo huo, pia kocha wa makipa, Mfaume Athuman naye anadai mishahara ya miezi miwili Aprili na Mei.

Akiongea na Mwananchi, Minziro alisema: "Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kuhusu kibaruachangu Yanga, nasubiri kwanza tukutane na uongozi wiki ijayo, kabla ya kuchukua uamuzi mwingine."

"Siwezi kwenda kuifundisha timu pasipo kulipwa haki yangu, nafikiri napaswa kulipwa kwanza jasho langu ndipo tufanya makubaliano mengine mapya."

Mtendaji Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa alikiri madai ya makocha hao kutolipwa mishahara, lakini akasema uongozi unaandaa malipo yao haraka ili waweze kuiandaa timu kwa ajili ya michuano hiyo ya Kombe la Kagame.
"Nikubali kwamba tuna madai yao, kinachoendelea kwa sasa ni kuhakikisha wanalipwa mapema na kuendelea na programu ya mazoezi," alisema.

Kikosi cha Yanga kinatarajia kuingia rasmi kambini Juni 14.Akiongea jijini Dar es Salaam jana, Shamte alisema yeye kwa sasa ni mchezaji halali wa Yanga na ataendelea kuvaa jezi za Kijani na Njano mpaka mkataba wake utakapokwisha Juni mwakani.

"Sina taarifa toka wa uongozi kwamba napelekwa kwa mkopo Toto, lakini kama huo ndiyo mpango wao, basi nawaeleza wazi kwa sitakuwa tayari kufanya mazungumzo ya kuondoka kwa mkopo kwa sababu nina imani bado kiwango changu kiko juu," alisema Ally.

Wakati huohuo, Kamati ya Usajili Yanga inatarajia kuweka wazi wachezaji watakaowaacha msimu huu wiki ijayo, huku ikisajili nafasi ya ulinzi na ushambuliaji.Ofisa habari wa Yanga Louis Sendeu alisema kuwa nafasi hizo mbili ndizo zilizokuwa kiini cha kufanya vibaya msimu huu kwa timu yao.

Kamati ya usajili ya Yanga inaundwa na Abdallah Bin Krebu, Seif Mohamed, Musa Katabalo na mdhamini wao.
"Kamati inakamilisha majina ya wachezaji watakaoacha na wakati wowote wiki ijayo tutaweka wazi majina ya wachezaji wa kuachwa ili watafute timu nyingine,"alisema Sendeu

Baadhi ya wachezaji wanaotajwa kuachwa ni Shedrack Nsajigwa, Davis Mwape na Abuu Ubwa.

Posted by Unknown on 8:34 AM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added