|

Makala: AY na B’Hits na urafiki uliochuja kimya kimya



Kwa muda mrefu sana Hermy B, CEO wa B’Hits Music Group na Ambwene Yesaya aka AY walikuwa maswahiba zaidi ya chanda na pete. 
Uhusiano wao ulikuwa na mafanikio kwa kila mmoja. Nyimbo kama habari ndio hiyo, nangojea ageuke, Leo, Bed and Breakfast na nyingine nyingi zake AY zilitengenezwa ba Hermy B ambaye pia ni jaji wa mashindano ya Tusker Project Fame. 
Kabla ya nyimbo hizo ni wachache sana waliokuwa wanamjua Hermy B. Ni wazi kuwa AY alimtambulisha Hermy kama miongoni mwa watayarishaji wazuri nchini Tanzania.
Lakini hivi karibuni kumekuwepo na fununu kuwa ushkaji kati ya nguli hao umefikia tamati. Tweet hii iliyoulizwa kwa AY na mdau mkubwa wa leotainment @Haile19 leo (May 23) ikatupa jibu la maswali yetu kuhusiana na tetesi hizo “ni kweli ur not with #Bhitz anymore!” ambapo AY amejibu moja kwa moja “YES”
Mashaka kuhusiana na uhusiano wao yalianza kuonekana baada ya AY kuwa na mpango wa kwenda kufanya video nchini Afrika Kusini akiwa na producer wa Mj records, Marco Chali ambaye ndiye aliyeutengeneza wimbo huo. Na jana (May 22) wamewasili mjini Johannesburg kwa ajili ya shughuli hiyo.

Wakati wa urafiki kati ya AY na Hermy hakuna kazi ambayo AY alikuwa akiifanya nje ya usimamimizi wa Hermy. Uamuzi wake wa kwenda kufanya kazi MJ Records ukaashiria kuwa uhusiano wao umeingia matatani. Kuna maneno pia sababu za kuvunjika kwa ushkaji huo umetokana na tamaa ya Hermy B ambaye alidaiwa kumtaka AY aanze kumlipa producer huyo shilingi milioni 10 kwa wimbo mmoja.
Kwa wengi kitendo hicho kinaonesha wazi kuwa Hermy alianza kuingiwa na kinyongo na kuona kuwa analipwa kiasi kidogo licha ya AY kufanya show nyingi ndani na nje ya nchi zinazomlipa sana. Kwa kawaida kama huo ni ukweli basi Hermy alikuwa sahihi kwamba kwanini umlipe laki 4 ama tano kwa single moja wakati wewe unaingiza zaidi ya milioni 20 kwa wiki moja ama mbili (makadirio).
Hata hivyo shilingi milioni kumi kama tozo ya wimbo mmoja kwa Tanzania bado haiwezi kuwaingia akilini wasanii wengi hata wale wenye kipato kikubwa akiwemo AY.
Sababu nyingine ya wazi kabisa kuwa AY na Hermy si ‘wana’ tena ni ukaribu wa hivi karibu kati yake na Master J ambao bila shaka umetokana na uswahiba wa Master J na Salama Jabir ambao nao ulitokana na kuwa majaji wa Bongo Star Search. Pamoja na kuwa Master J na AY wanafahamiana tangu siku nyingi kama msanii na producer, tunahisi kuwa ushirikiano wa AY na Salama Jabir katika kuanzisha kipindi cha TV cha Mkasi kimewaweka karibu zaidi Master J na AY kwa kupitia Salama. 
Sababu ya tatu iliyotufanya tutilie shaka uhusiano wa B’Hits na AY, ni kile alichokisema Hermy B na kuandikwa hapa mwanzoni mwa mwezi huu kuwa hakuna msanii tajiri Tanzania.

Kauli hii ya Hermy ilitupa mashaka na kuiona kuwa huenda imetokana na kitu kinachomuumiza moyoni hususan mafanikio ya AY ambaye wengi tunaamini ni miongoni mwa wasanii matajiri nchini Tanzania.
Hata kama AY na Hermy B (B’Hits) wakiendelea kutokokuwa karibu kimuziki, walipofika wote si pa kubeza na kutokana na ubunifu, kujituma na uwezo wao binafsi kila mmoja ataendelea kupata mafanikio katika upande wake na maisha yanaendelea

Posted by Unknown on 12:32 PM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added