|

Upelelezi kesi ya Lulu bado haujakamilika

UPELELEZI wa kesi ya mauaji inayomkabili muigizaji nyota wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu bado haujakamilika.Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. 

Lakini jana Wakili wa Serikali, Peter Sekwao aliieleza mahakaama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine.Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando aliahirisha kesi hiyo na hadi Juni 18, 2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Hata hivyo, jana mshtakiwa huyo alilazimika kupandishwa kizimbani mara mbili baada ya tarehe ya kutajwa tena kukosewa.

Awali, hakimu Mmbando alisema kuwa kesi hiyo ingetajwa tena Juni 28 kisha mshtakiwa huyo akaondolewa mahakamani na kupelekwa mahabusu akisubiri kurejeshwa mahabusu ya gereza la Segerea.
Lakini baadaye alirudishwa tena mahakamani na kupandishwa kizimbani baada ya kubainika kuwa tarehe iliyopangwa ya kutajwa kwa kesi hiyo haikuwa sahihi kwani karani alikuwa amekosea kuhesababu, ndipo ikapangwa Juni 18.

Jalada hilo lilipelekwa Mahakama Kuu Ijumaa ya Mei 18, mwaka huu baada ya jopo la Mawakili wa mshtakiwa  huyo kuwasilisha maombi juu ya uchunguzi kuhusiana na umri halali wa msanii huyo.

Umri wa mshtakiwa huyo umezua utata kama ni mtoto au ni mtu mzima, jambo ambalo limewalazimu mawakili hao kuwasilisha maombi hayo ya uchunguzi wa umri wake Mahakama Kuu.Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili Peter Kibatala Mei 15, 2012 na yamepangwa kusikilizwa  na Jaji Dk Fauz Twaib Mei 28, 2012.

Mawakili wa mshtakiwa huyo walifikia uamuzi wa kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu baada ya kugonga mwamba Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kabla ya kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu, mawakili hao waliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 7,2012  wakiiomba iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto wakidai kuwa bado ni mtoto.

Mawakili hao walidai mahakamani hapo kuwa msanii huyo ana umri wa miaka 17 na kwamba kwa maana hiyo yeye bado ni mtoto na kesi yake haipaswi kusikilizwa katika mahakama za kawaida kama mtu mzima. 
Kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea msanii huyo, wakili Kenedy Fungamtama alidai kuwa mteja wao ana umri wa miaka 17 na si 18 kama inavyotamkwa mahakamani.

Alidai kuwa hata cheti cha kuzaliwa walichokiwasilisha mahakamani kinaonyesha mahali na tarehe aliyozaliwa mshtakiwa hivyo kuwa na umri wa miaka 17.

“Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatafsiri kuwa mtoto ni yule aliyekuwa na umri chini ya miaka 18 hivyo katika suala la mteja wetu alipaswa kushtakiwa katika mahakama ya watoto,” alidai Wakili Fungamtama.

Hata hivyo upande wa mashitaka kupitia kwa wakili Elizabeth Kaganda ulipinga maombi hayo na kudai kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo na hivyo kuomba wapewe muda zaidi.
Wakili Kaganda pia alidai kuwa hata jina linaloonekana katika cheti cha kuzaliwa cha mshtakiwa huyo linasomeka kama Diana Elizabeth wakati mshtakiwa huyo ametajwa mahakamani hapo kama Elizabeth Michael.

Akijibu hoja hiyo, wakili Fungamtama alikiri jina hilo kusomeka Diana Elizabeth na kusema kuwa ni jambo la kawaida hasa kwa wakristo kuwa na majina mawili.
Katika uamuzi wake, Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo alisema kesi hiyo bado iko kwenye upelelezi na kwamba kulingana na jinsi ilivyo isingekuwa busara kuamua hoja yoyote.
Hivyo Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo, aliutaka upande wa utetezi uwasilishe maombi hayo kupitia Mahakama Kuu.

Katika maombi  namba 46 ya mwaka 2012, mawakili hao wanaomtetea msanii huyo wanaiomba Mahakama Kuu itoe uamuzi kama Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kuamua ufanyike uchunguzi wa umri halali wa msanii huyo.

Jopo la mawakili hao maarufu linadai kuwa linaamini kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo kwa sasa ndio bado inayoshughulikia kesi hiyo, ina mamlaka ya kufanya au kuamuru ufanyike uchunguzi wa umri mshtakiwa huyo. 

Lakini pia wanaiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo huo, basi Mahakama Kuu yenyewe ifanye uchunguzi huo.

Akifafanua juu ya maombi hayo Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS) alisema kuwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kifungu cha 113 inaruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa.

Wakili Kibatala alisema lengo la uchunguzi huo ni  ili mahakama iweze kujiridhisha kama mshtakiwa ni mtoto au ni mtu mzima kwa lengo la kujipa angalizo juu ya maslahi ya mtoto.

“Baada ya uchunguzi huo mahakama ikijiridhisha kuwa ni mtoto basi mwenendo wa kesi hiyo utaendeshwa kwa maslahi ya mtoto kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria hiyo ya mtoto,” alisema Wakili Kibatala.

Kwa mujibu wa Wakili Kibatala kifungu hicho ambacho huelezea ulinzi wa maslahi ya mtoto katika uendeshaji wa kesi kwa watoto wanaokinzana na sheria.

Mbali na Kibatala na Fungamtama ambaye pia anaitetea Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans dhidi ya Tanesco, mawakili wengine katika jopo hilo ni Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo.

De-Melo ambaye amewahi kuwa Rais TLS, pia ni mshindi wa  wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King. 

Jopo la mawakili hao wanaomtetea msanii huyo linahitimishwa na Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Posted by Unknown on 12:11 AM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added