|

Rais Amteua Wakili wa Lulu Kuwa Jaji



RAIS Jakaya Kikwete amemwapisha kuwa Jaji wakili wa kujitegemea, Joaquine De-Mello ambaye alikuwa akimtetea msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu)  anayetuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Wakili huyo, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King ya mwaka 2012 na ambaye alikuwa pia alikuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) ni miongoni mwa majaji 10 walioapishwa jana na Rais Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
De-Mello ni miongoni mwa mawakili wanne waliojitokeza Aprili mwaka huu kumtetea Lulu katika kesi hiyo ya mauaji inayomtuhumu kumuua usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu.

Mawakili wengine wanaomtetea Lulu ambaye umri wake umekuwa na utata ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.

Akizungumza kwenye viwanja vya Ikulu, De-Mello alisema baada ya kuteuliwa kuwa Jaji, sasa atafanya kazi hiyo na moja ya mikakati yake ni kukabiliana na changamoto za wingi wa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Majaji wengine walioapishwa jana na Rais Kikwete ni Francis Mutungi, John Mgeta, Patricia Fikirini, Sam Rumanyika, Salvatory Bongole, Jerald Alex, Mathew Mwaim, Jacob Mwambegele na Latifa Mansook.
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman alisema amefurahi kuteuliwa kwa majaji hao na anawafahamu kuwa wote ni wazoefu na watatekeleza kazi zao kikamilifu.

“Wote ni wazoefu. Ukiangalia utaona kuwa sita walikuwa wakifanya kazi mahakamani (Mahakama Kuu na Rufani), wawili mawakili wa kujitegemea na wawili pia mawakili wa Serikali,” alisema Jaji Othman.
Alisema majaji hao wote kabla ya kupangiwa kazi rasmi itabidi waanze kufanya kazi ya kukabiliana na kesi zaidi ya 2,200 zilizopo katika Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi.

Uteuzi wa majaji hao 10, alisema unaifanya Mahakama Kuu sasa kuwa nao 69 tofauti na wale 16 wanaounda Mahakama ya Rufani.
Othman alisema pamoja na uteuzi huo wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kulundikana kwa kesi nyingi kuliko uwezo wao.
“Walioteuliwa watasaidia lakini ukweli ni kwamba bado tunakabiliwa na upungufu wa majaji. Kesi ni nyingi,” alisema Othman.

Hakuweza kueleza mara moja idadi kamili ya majaji inayotakiwa ili kukidhi mahitaji lakini akasema kuwa Serikali imeliona hilo na imekuwa ikilifanyia kazi hatua kwa hatua.

Licha ya upungufu wa majaji, Jaji Othman alisema wanakabiliwa na tatizo la kutumia teknolojia ya zamani ya kusikiliza na kuandika tofauti na maendeleo ya sasa ambayo yanahitaji kurekodi.
“Mfumo huu wa kutumia teknolojia ya kisasa pia ungeweza kuharakisha kesi,” alisema Jaji Othman lakini akasema Kitengo cha Biashara tayari kimeanza kuifanyia kazi teknolojia ya kisasa.

Kwa kutumia teknolojia hiyo, alisema mtu anaweza kutumia simu yake ya mkononi kujua siku ya kesi yake na hata kuperuzi kwenye mtandao kupata hukumu pamoja na mwenendo wa kesi yake. 
Alisema wanatarajia kwenda hatua kwa hatua ili kuhakikisha teknolojia hiyo ya kurahisisha kazi za mahakama inaenea idara zote za Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Majaji wengine wapya nao walisema kwenye mahojiano na waandishi wa habari kwamba moja ya changamoto ni kufanya kazi katika mazingira magumu na wingi wa kesi zilizolundikana katika mahakama hiyo.
Jaji Mutungi alisema yeye anaamini kiu kubwa ya Watanzania ni kupatiwa haki na kwamba haki hiyo inapocheleweshwa pia ni tatizo jingine.

Ili kuhakikisha anawatekelezea Watanzania haki zao, Mutungi alisema atajitahidi kufanya kazi kwa bidii na kumaliza kesi nyingi kwa haraka.

Kwa upande wake, Jaji Mgeta alisema pamoja na wingi wa kesi kazi kubwa wanayopaswa kuifanya ni kuwa waadilifu na watenda haki.

Alikiri kwamba Tanzania wako nyuma katika teknolojia ya kuendesha kesi lakini akasema hilo halipaswi kuwa ni jambo ambalo litawafanya warudi nyuma na kutotekeleza wajibu wao kikamilifu.

Posted by Unknown on 1:47 AM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added