|

Domayo: Nililazimishwa kupiga penalti

"Usisikie kwenda kupiga penalti...siku zote sitaki kusikia suala hili, kwani pale ni ufundi tu sasa ukikosea kwa kupiga nje au kumlenga kipa, lawama ndugu yangu" anasema Frank Domayo chipukizi wa JKT Ruvu aliyejiunga na Yanga alipokuwa akiitumikia Taifa Stars Msumbiji.

Domayo alifunga penalti ya saba katika mchezo uliomalizika kwa Stars kufungwa penalti 7-6 na Msumbiji katika mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini baadaye mwakani. Mechi hiyo ilipigwa Uwanja wa Taifa Zimpeto jijini Maputo.
"Nililazimishwa kwenda kupiga penalti baada ya wachezaji wengine kuogopa...mimi siyo mpigaji mzuri wa penalti kwa hiyo baada ya Boko (John) kupiga penalti ya sita na kupata na Msumbiji nao wakapiga wakapata, kila mtu aliogopa kwenda kupiga.
"Ngassa (Mrisho), Samatta (Mbwana) na Haruna (Moshi) wote walikataa wakanilazimisha mimi kwenda kupiga, nikasema poa tu ngoja nikajaribu lakini huku miguu ikinitetemeka.
"Wakati ninakwenda nikawaza, Watanzania wote wananitazama mimi, hizi ndiyo lawama zenyewe ukikosa. Nilipanga nipige upande wa kulia sikubadili uamuzi,  nashukuru Mungu nilifunga.
"Nikawaangalia Ngassa na Boban...Ngassa akaenda kupiga penalti ya nane akapata jamaa wakapata, sasa ikabakia kwa Samata na Haruna wakawa wanasakiziana kwenda kupiga."Mbwana akamwambia Kaseja piga hiyo, lakini naye akasita basi Samatta akaenda kupiga kwa bahati mbaya alikosa kwa kipa kuipangua.
"Kaka ile ni presha tupu, ukisikia mashabiki wanakuzomea wakati unakwenda kupiga penalti unahitaji umakini na utulivu wa hali ya juu kufanya kile unachotaka," alisema Domayo.
Waliopata penalti kwa Stars ni Amir Maftah, Shabaan Nditi, Shomari Kapombe, John Boko, Frank Domayo, Mrisho Ngassa wakati waliokosa ni Aggrey Morris, Kelvin Yondani na Mbwana Samata.
Lakini kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesifu uwezo wa kujituma ulioonyeshwa na wachezaji wake katika mchezo wao wa juzi dhidi ya Msumbiji na kusema: "Wachezaji wangu walicheza vizuri na kujituma kama nialivyotaka.
"Najivunia wachezaji wangu walifanya kile nilichotaka, lakini bahati haikuwa yao inapofika suala la penalti huwa hakuna mwenyewe kwani hata timu kubwa Ulaya zinatolewa.
"Jambo zuri zaidi ni kwamba tumekuja hapa na kufunga mabao kama tulivyowahidi wa Tanzania, kwamba tunakwenda Msumbiji tutapata bao ndicho tulichofanya tena tumepata mabao saba.
Kim aliwapongeza wenyeji kwa kutumia vizuri nafasi yao ya kuwa nyumbani na kupata ushindi huo.
Naye nahodha wa Stars, Juma Kaseja alisema bahati haikuwa yao, lakini sasa ni wakati wa kujipanga upya.

"Timu ni nzuri, tumecheza mechi nne sare moja na Malawi, tukafungwa na Ivory Coast na tumeshinda Gambia kabla ya kufungwa Msumbiji. Nadhani wote mmeona mabadiliko."
"Watanzania wanatakiwa kuwa na subira ili timu iendelee kujiamini kwa sababu kuna wachezaji wengi ni chipukizi na wengi wanacheza vizuri," alisema Kaseja. Naye beki Kelvin Yondan alisifu jinsi walivyojituma na hata kusawazisha bao japokuwa wametolewa kwa mikwaju ya penalti.

Posted by Unknown on 11:55 PM. Filed under , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added