Skendo ya Kutumia Madawa ya Kelevya-Uwoya , Janet Hapatoshi
Na Musa Mateja
Skendo ya matumizi ya dawa za kulevya imesababisha mastaa wawili wa filamu za kibongo, Irene Pancras Uwoya na Janet Mathias kuingia kwenye bifu zito na sasa hapatoshi huku kila mmoja akianika siri nzito za mwenzake, Risasi Jumamosi linafunguka.
Wiki mbili zilizopita, Uwoya ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunguka kupitia gazeti hili kuwa alifikia hatua ya kusitisha urafiki wake na Janet kwa madai kuwa alikuwa na skendo hiyo.
UWOYA AIBUA SKENDO
Katika mazungumzo yake yaliyokuwa hayaandikiki gazetini, Uwoya alimsiliba Janet kwa kuanika siri zake nzito, jambo ambalo lilimpandisha hasira msanii huyo na kujikuta naye akimjibu kwa kumchana kama yeye alivyofanya.
Muda mfupi baada ya Uwoya kumwanika, Janet alizama mtandaoni akamlipua mwenzake kuwa alikuwa akiishi naye nyumbani kwao lakini ilishindikana kwa kuwa alikuwa ‘anabwia unga’.
HUYU HAPA JANET
“Huyo anayejiita…(tusi) Irene Uwoya hawezi kuniharibia jina langu kwenye jamii. Anasubiri nikiwa nje ya nchi ndiyo anaanza kusambaza habari mbaya zinazonihusu. Kwa nini asinitafute uso kwa uso?,” ilisomeka sehemu ya mapigo ya Janet ambayo alithibitisha kuwa yanapatikana kwenye ukurasa wake.
UWOYA NAYE
Kwa upande wake, Uwoya alipopatikana tena, alisisitiza kuwa anachofanya Janet ni kumchafua katika jamii kwa vile yeye ni mtu anayeheshimika. Akasema kuwa kamwe hawezi kutumia unga.
HUKO NYUMA
Uwoya na Janet ni marafiki wa siku nyingi ambao walianza kutibuana hivi karibuni baada ya Janet kuingia kwenye filamu akidaiwa kupindua ndoa ya mwenzake.