UTABIRI MZITO...
SIKU kadhaa baada ya kifo cha Steven Kanumba, mtu mmoja aliyedai kuwa ni mwanachama wa jamii ya Freemason (Waashi Huru), Charles Willbard ametabiri mambo mengi mazito na ya kutisha akidai yatotekea nchini.
Katika mahojiano maalum na Uwazi hivi karibuni, mtu huyo aliyedai kuwa alikuwa ni msimamizi katika taasisi hiyo kabla hajajiuzulu alisema kuwa kama ilivyotokea miujiza katika mazishi ya staa huyo, wanawake wote wanaozimia katika misiba ya mwanachama wa Freemason wategemee kujifungua watoto wa ajabu baada ya miezi tisa tangu msiba kutokea.
Alisema kwenye misiba ya wanachama wa taasisi hiyo wanaozimia huwa wanavalishwa vitu vya kishetani bila wao kujijua ndiyo maana wanadondoka na kuzimia.
Kwa upande mwingine mtu huyo alisema kuwa wale wote wanaovaa tisheti zinazokuwa na picha ya marehemu ambaye ni mwanachama wa taasisi hiyo msibani nao huwekewa alama na baada ya muda huota ndoto mbaya.
Alipoulizwa dawa ya tatizo hilo alisema kwamba dawa pekee ni kuomba kila mtu kwa dini yake na wakifanya hivyo watakuwa wameondokewa na ndoto hizo.
Alisema kuwa wanaoweka mashada ya maua na kutupa udongo katika kaburi la mwanachama wa Freemason kama siyo wafuasi wao wanakuwa na bahati na kufaidika hasa wasanii wenye majina kwani baadaye wanaachana na usanii na kufungua miradi mingine mikubwa.
Aliongeza kuwa wale wanaofanikiwa kumzika mwanachama wa taasisi hiyo kwa kuingiza kaburini jeneza lake, hupata utajiri wa fedha na mafanikio kazini na katika biashara zao.
Mshiriki huyo ambaye alijiunga na Freemasons Januari mosi, 2009 jijini Mwanza baada ya kushawishiwa na Mwarabu mmoja kutoka Dubai alibainisha kuwa alikubali kujiunga baada ya kuelezwa kwamba ataishi kama mfalme.
Alidai kwamba alipakwa mafuta ya aina fulani, akapewa mkufu na pete alizofaa na akaanza kupata fedha nyingi.
Alieleza kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu alifanikiwa kupata zaidi ya shilingi milioni 216,000,000 lakini cha kushangaza kwa sasa amekuwa akiota ndoto za ajabu na kuteseka hali iliyomfanya atupe vitu hivyo baharini na baada ya kufanya hivyo fedha zilianza kupotea.
“Natarajia kubadilika na kuingia katika dini ya Kikristo, masharti ya hawa watu ni magumu sana ingawa nimefaidika kwa kutembelea nchi nyingi kama Kenya, Uganda, Rwanda na nilipata mialiko 21 ya hapa Tanzania lakini sasa naachana nayo,” alisema.