Mkwasa:Wasagaji tuliwatimua Twiga Stars
Mkwasa alitangaza kuachia ngazi kuifundisha Twiga mwanzoni mwa wiki hii ikiwa ni siku moja baada ya kukosa fursa ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kufuatia kufungwa nyumbani na ugenini na wenzao wa Ethiopia.
Mkwasa, mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Yanga na timu ya Taifa (Taifa Stars), alikiri kuwapo kwa vitendo hivyo kwa baadhi ya wachezaji, na waliobainika walichukuliwa hatua mara moja.
Bila kuwataja majina baadhi ya wachezaji waliokuwa na tabia hizo, Mkwasa alisema uongozi wake ulilazimika kuwatimua waliobainika kupenda mchezo huo.
Mkwasa aliyekuwa akihojiwa na kipindi cha 'Tuongee asubuhi' kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Star Tv alisema: “Kwa wale tuliokua tukiwasikia na kupata ushahidi kupenda tabia ya usagaji tuliwaondoa kwenye timu."
Mkwasa alisema mara kwa mara alikuwa akiwasiliana na meneja wa timu kufuatilia kwa karibu tabia za wachezaji hao.
“Nilikuwa nawasiliana na meneja wa timu na kuchukua hatua haraka kwa wale wote waliokuwa na tabia ya kupenda kusagana," alisema kocha huyo.
Wakati huohuo, mdau mkubwa wa soka la wanawake nchini na miongoni mwa waanzilishi wa ligi ya wanawake jijini Dar es Salaam, Frank Mchaki, amepongeza hatua ya aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa (Twiga Stars), Boniface Mkwasa kuachia ngazi.
Mchaki, alisema uamuzi wa Mkwasa unastahili pongezi hasa kutoka na ukweli kwamba siyo utamaduni wa wengi kukubali kuwajibika pale wanaposhindwa kufikia malengo waliyopewa.
"Nampongeza kwa uamuzi wake, lakini Chama cha Soka la Wanawake (TWFA), ambacho ndicho chenye jukumu la kuhakikisha soka la wanawake linasonga mbele kinafanya nini,"alihoji Msaki.
Mchaki, Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Kindondoni (Kifa), alisema ni ndoto kwa soka la wanawake kufanikiwa kama hakutakuwa na mpango endelevu wa kuibua vipaji vipya.
"Timu yetu ni ile ile, wachezaji ni walewale miaka nenda, rudi. Sasa katika hali kama hii, Mkwasa anaweza kuleta mabadiliko?" alihoji Mchaki.
Matokeo ya kufanya vibaya kwa Twigani kwa sababu ya kutotiliwa mkazo ligi ya wanawake ambayo ndiyo mhimili mkubwa wa kujenga timu imara ya taifa.
Alitoa ushauri kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kukaa chini na kujadili kwa pamoja nini kifanyike ili kuinua soka hilo lililoanza kuvuta hisia za mashabiki wengi.
"Kwa hali ilivyo sasa, kufikia mwaka 2015, Twiga Stars hii tunayoiona sasa haitakuwapo tena kama hakutakuwa na juhudi za haraka kutoka mamlaka zinazosimamia mchezo wa soka," alisema Mchaki.