|

MAMA WEMA KICHEKESHO



MAMA wa Wema Isaac Sepetu, Mariam Sepetu ametoa kichekesho cha mwaka baada ya kufanya mahojiano na Tv moja ya jijini Dar akilenga kumsafisha mwanaye kwa kuwananga marafiki na magazeti pendwa, Ijumaa lina ripoti kamili.
Katika mahojiano hayo, Mama Wema ‘alibwabwaja’ mengi huku akitupia lawama makundi mengine wakiwemo marafiki wa kiume wa mwanaye.
AJISIFU KUMLEA WEMA VIZURI
Bila soni wala aibu, mzazi huyo alijisifu kumlea VIZURI Wema, jambo lililoibua maswali miongoni mwa watazamaji wa runinga hiyo huku wengine wakiomba kamusi ya Kiswahili sanifu ili kujua maana ya neno ‘vizuri’.
“Japo sikumnyonyesha lakini mwanangu nimemlea vizuri. Ana maadili mazuri ya Kiafrika,” alisema mama huyo.
AFUNGUKA BILA BREKI
Katika mahojiano hayo aliyoyafanya Juni 19, mwaka huu, mama huyo aliwashushia lawama mashoga wa mwanaye akisema walimpoteza Wema kwa kumpeleka kwa waganga wa kienyeji kipindi cha nyuma na kumfanya awe ‘mawengemawenge’.
“Nimehangaika sana usiku na mchana kumfanya mwanangu arudi kwenye hali yake ya kawaida. Marafiki zake walimpoteza, walimpeleka kwa waganga kitendo ambacho kilichangia kwa kiasi kikubwa kumpoteza mwanangu, akawa mtu asiyejielewa,” alifunguka bila breki.
ALIKOROGA, ATALINYWA
Kwa kauli hizo tu, Ijumaa lilipokea simu nyingi kutoka kwa mastaa na wasomaji wa kawaida wakidai kuwa mama huyo alikuwa amewachekesha kwani tangu kipindi hicho kilipokwenda hewani siku hiyo, marafiki wote wa Wema waliamua kujichenga na kumwachia maisha ya peke yake huku wakidai kama anataka kuishi kwa raha atafute kisiwa cha kuishi huko.
“Mdomo uliponza kichwa, sisi ni marafiki zake na tunafanya naye kazi kwa upendo mkubwa lakini kwa kauli ya mama tunaonekana tunajipendekeza. Acha aishi dunia ya peke yake,” alisema mmoja wa waigizaji kiwango hapa Bongo.

TURUDI KWA MAMA WEMA
Akiendelea kuropoka mambo bila kuanika ushahidi wa wazi, mama huyo alisema marafiki wote wa Wema ni wanafiki na kama mwanaye anataka marafiki wa kweli, ni yeye mama, dada yake Wema (pengine yule anayeishi Kumekucha- Sinza) na ndugu wengine wa karibu.
ETI WEMA MAMBO SAFI
Mama Wema alifunguka kuwa katika kipindi hiki ambacho mwanaye mambo yake yanamwendea vizuri hataki marafiki wanafiki wanaomfuatafuata Wema kwa lengo la kumchafua.
SNURA ACHAFUKA
Awali kabla mama Wema hajaanza kutiririka runingani, msanii wa filamu Snura Mushi aliongea akisema yeye na Wema ni marafiki wakubwa mpaka watu wanamsema vibaya kwamba, amekuwa mpambe wa Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006.
Snura akasema wao wanapendana sana, watakuwa sambamba hadi siku kila mmoja atakapoishi maisha mengine. Wema naye alikazia hapo kwa kukiri yeye na Snura ni marafiki wakubwa.
Lakini mama Wema alipopewa muda wa kuwa hewani, alimchana hadi Snura kwamba ni walewale. Hebu msikie:
“Mwanangu Wema, nakwambia mimi mama yako, jihadhari na marafiki wanafiki. Rafiki wa kweli ni yule anayekujali, wengine wanafiki. Haohao ndiyo wanaokucheka ukiandikwa vibaya kwenye magazeti, wewe huna rafiki wa kweli.”
HIVI ALIJIULIZA HILI SWALI?
Kwa mujibu wa wadau wengi waliopiga simu kwenye dawati la Ijumaa walihoji kwa nini mzazi huyo hakuanika chanzo cha utajiri wa Wema na kumhoji mwanaye alikopata Sh. milioni 400 za kununulia nyumba (ingawa imebainika si yake) kwani hana filamu aliyocheza ikamwingizia mkwanja huo wote.
WOLPER NAYE HAKUWA SALAMA
Katika tuhuma hizo, mama Wema alimshambulia mwigizaji Jacqueline Wolper akidai alimkosea mwanaye (kipindi hicho alichopotea) kwa kumwambia kuwa amchezeshe filamu moja ili amlipe fedha ya kwenda kununua kitanda wakati yeye anaamini mwanaye kamwe hajawahi kukumbana na tatizo la kukosa mahali pa kulala katika maisha yake.
KITUKO
Wakati akihojiwa, mama huyo alionesha kitanda kipyaaa na cha kisasa akidai ndicho alichokuwa akilalia Wema tangu akiwa mdogo hadi leo ana miaka 23. Hata hivyo, kitanda hicho kilionekana kama kimenunuliwa jana yake.
WOLPER ASHINDWA KUJIZUIA, AMJIBU MAMA WEMA
“Mh! Sijui ataelewekaje huyo mama na tena kwa bahati mbaya huwa sitazami hizo local channel (televisheni inayotazamwa na eneo fulani pekee) ambazo nasikia ndiyo ametumia kunizungumzia na kunishirikisha mimi na mwanaye. Mimi huwa natazama DSTV. Niliambiwa na watu walioona.”
AORODHESHA WANAUME WA WEMA
Akitambaa na msururu wa wanaume waliotoka kimapenzi na mwanaye (bila kujali kuwa siyo maadili kwa binti wa Kiafrika), mama Wema alisema ni kweli mwanaye ‘amesharukaruka’ na vijana wawili watatu.
Aliwataja marehemu Steven Kanumba (alithibitisha alijua) kuwa alikuwa miongoni mwa wanaume wa Wema huku akimshukuru na kumuomba Mungu amrehemu huko mbele za haki aliko.
Pia mzazi huyo alimtaja mjasiriamali, Jumbe Yusuf Jumbe na kumalizia na mwanamuziki mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdu Juma ‘Diamond’ kuwa hao ndiyo wanaume wa Wema pekee.
Majina hayo siyo mageni kwani ni yaleyale yaliyokuwa yakichorwa na magazeti pendwa ingawa alimsahau mwanamuziki wa Mashujaa Band, Charles Gabriel ‘Chaz Baba’ huku Wema mwenyewe akiomba majina ya wasanii Khaleed Mohamed ‘TID’ na Herry Samir ‘Mr Blue’ yakatwe kwenye listi.
MTITI KWA DIAMOND
Mariam alipofika kwenye jina la Diamond, ndipo akawaka si kitoto akidai kuwa hakuwahi kumtarajia kama anaweza kuwa mkwewe hata siku moja kwani ni mpuuzi na mhuni.
“Mtu wamekutana tu huko, bila kushirikisha wazazi anamvalisha pete kwenye klabu za muziki. Nilishajua mwisho wake sababu ni mhunimhuni tu aliyemtumia mwanangu kama daraja la kupandia afike anakotaka.”
LAKINI TUJIKUMBUSHE
Wakati Wema anamtongoza Diamond kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook mwaka 2010, tayari ‘kichaa’ huyo wa Bongo Fleva alikuwa juu kwani tayari alishavunja rekodi kimuziki kwa kutwaa tuzo tatu za Kili hivyo si kweli kwamba alitaka umaarufu.
FAMILIA YA DIAMOND
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na familia ya Diamond kilipenyeza habari kuwa, hawakufurahiswa na kitendo cha mama Wema kulipuka runingani kwani hata mama Diamond naye ana uwezo wa kufanya hivyo.
WEMA VIPI?
Baada ya kipindi hicho kwenda hewani, Wema aliwasiliana na chumba chetu cha habari akilia na kuhaha kuwa mama yake alikuwa amezungumza vitu ambavyo hata yeye hakutarajia (meseji zake tunazo).
ONYO LA MAGAZETI PENDWA
Katika kipindi hicho, mama Wema alipigilia msumari wa mwisho pale alipoyapa mwezi mmoja magazeti pendwa yaache kumwandika mwanaye.
“Haya magazeti ya udaku (pendwa) nayapa mwezi mmoja kuanzia leo hii ninavyoongea, yaache kumwandika mwanangu, safari hii wajue hawadili na Wema, wanadili na mimi mama yake.
“Wewe Shakoor wewe, Shakoor (Jongo). Si unajifanya upo karibu sana na Wema kumbe mnafiki mkubwa, nilishawahi kukupopoa mawe, hujakoma, sasa marufuku kwa mwandishi yeyote kuja hapa nyumbani kwangu.”
MEZANI KWA MHARIRI
Mama Wema ana uhuru wa kuzungumza kama walivyo Watanzania wengine, ameshatoa yake ya moyoni, sasa awaachie wengine nao ni zamu yao.

Posted by Unknown on 11:47 PM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added