Lowassa:" Nasema Hawaniwezi"
Moses Mashalla, Arusha, Raymond Kamnyoge, Dar
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amewapiga vijembe aliowaita maadui zake kisiasa wanaomchafua katika majukwaa mbalimbali akisema kuwa, hawamuwezi na hawamnyimi usingizi.
Lowassa akitambia maadui zake, kambi yake nayo imezidi kujizatiti baada ya mshirika wake kisiasa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge amefanikiwa kukalia kiti cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi hivyo kuzidi kuongeza nguvu kwenye bungeni.
Jana, akiwa mkoani Arusha katika harambee ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Elaira, Lowassa alitumia sehemu ya muda wake kuwapiga vijembe maadui zake pasipo kuwataja majina akisema kamwe hawamnyimi usingizi.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alitoa kauli hiyo, baada ya Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer kumtaka aendelee kufanya kazi ya Mungu licha ya baadhi ya watu kumkatisha tamaa.
Akizungumzia kauli ya Askofu Laizer, Lowasa alisema mahasimu wake kisiasa wamekuwa wakimsema kupitia vyombo mbalimbali vya habari, lakini akatamba kwamba juhudi hizo hazitaweza kufua dafu kwake kwani kelele zao hazimnyimi usingizi.
“Wanaonisema kwenye magazeti wala hawanisumbui, nasema hawaninyimi usingizi kwa kuwa mimi namtegemea yule anitiaye nguvu daima,” alisema Lowasa, kitendo kilichosababisha kushangiliwa na waumini waliohudhuria kanisani hapo.
Aliongeza kuwa yeye daima humtegemea Mungu amtiaye nguvu na kamwe hawezi kushindwa kulala usingizi kwa kusikiliza kelele zao za mara kwa mara.
“Nakushukuru Baba Askofu kwa kunijibia, wale wote wanaonisemasema kwenye magazeti wala hawanisumbui na wala hawaninyimi usingizi,” alisema Lowasa.
Alisema kwamba yeye ataendelea kumtumikia Mwenyezi Mungu ambaye amtiaye nguvu siku zote bila kujali maneno ya mahasimu wake wa kisiasa.
Kabla ya kuendesha harambee hiyo, Lowasa aliwaongoza waumini wa kanisa hilo kwa nyimbo zilizopo kwenye Kitabu cha Tenzi za Rohoni na kuibua shangwe kanisani hapo.
Kambi yake yajizatiti
Chenge ambaye ni mshirika mkubwa wa Lowassa kisiasa amechaguliwa katika kamati nyeti ya Bunge ya Fedha na Uchumi, akizidi kuongeza nguvu kwenye mhimili wa kambi hiyo.
Lowassa mwenyewe anaongoza Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama huku mshirika wake mwingine, Peter Serukamba akiongoza Kamati ya Miundombinu.
Katika uchaguzi wa juzi wa kamati hiyo uliotawaliwa na malalamiko ya vitendo vya rushwa bila kuelezwa ilikuwa ikitolewa na kambi ipi, aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti ni Dunstan Kitandula ambaye ni mbunge wa Mkinga.
Uchaguzi huo ulikuwa wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk Abdallah Kigoda aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda hivi karibuni.
Akizungumzia uchaguzi huo jana, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema, Chenge alipata nafasi hiyo baada ya kumshinda Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa.
“Mwambalaswa alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi kabla ya uchaguzi, hivyo aliamua kujiuzulu ili kugombea nafasi ya uenyekiti na Chenge, lakini akashindwa," alifafanua Dk Kashillilah.
Alipotakiwa kuzungumzia mizengwe na rushwa iliyotawala kwenye uchaguzi huo, Dk Kashililah alisema hawezi kuzungumzia hilo kwa sababu hakuwepo kwenye mchakato wa upigaji kura.
“Wanaoweza kuzungumzia hilo ni wale waliopiga kura ndiyo wanaweza kuelewa kama kulikuwa na mazingira ya rushwa lakini mimi sikuwapo,” alisema.
Tayari kambi ya Lowassa pia inaonekana kuwa na nguvu katika baadhi ya kamati kutokana na kuwa na washirika wenye msimamo wa wastani akiwemo Agustine Mrema wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) inayoongozwa na John Cheyo, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) inayoongozwa na Zitto Kabwe na hata Kamati ya Bunge ya Katiba ya Sheria na Utawala inayoongozwa na Pindi Chana