Bongo Star Search: Shindano linalotoa washindi wasiomudu ushindani wa muziki
Harufu inayodhihirisha kuwa mashindano ya mwaka huu yanaweza kuwa na utofauti mkubwa imeshaanza kunukia. Kwanza kwa matangazo yanayovutia yaliyoandaliwa na wadhamini, yanayosikika kwenye vituo vya radio na kuamsha hamu ya watazamaji wa TV wanayoyasubiria.
Kingine ni safari ya waandaaji na majaji wa show hiyo ya mjini Mumbai, India. Haijulikani wameenda kufanya nini hasa lakini inavyoonekana wameenda kutengeneza vipande kadhaa vya video vinavyohusiana na mashindano hayo kama si matangazo yenye gharama yatakayokuwa yakirushwa kwenye TV kwa hisani ya wadhamini.
Kama haitoshi mwaka huu BSS imekuja na kitu kiitwacho Marafiki wa BSS. Wamechaguliwa wanamuziki kumi wa hapa nchini watakaokuwa na kazi ya kuwafundisha ujuzi na masuala muhimu ya muziki washiriki watakaokuwa wamechaguliwa kutoka kwenye usaili katika mikoa mbalimbali na kuja kwenye kambi ya Dar es Salaam.
Miongoni mwa walimu hao ni pamoja na wanamuziki wakongwe King Kiki ambaye wimbo wake unasikika kutumika katika tangazo mojawapo la mashindano hayo, Juma Kakere na malkia wa Taarab nchini Patricia Hillary.
Wengine ni pamoja na Dully Sykes, Dito, Amin, Rachel, Barnaba, Mwasiti na Marlaw.
Pamoja na maandalizi hayo yanayoashiria kuwa wadhamini wamemwaga mshiko wa kutosha, historia inaonesha kuwa tangu BSS ianze imekuwa ikitoa washindi ‘vibogoyo’ wasioweza kukiuma kipande cha nyama cha muziki wa Tanzania kinachotafunwa zaidi na wasanii waliotoka kwa njia za kawaida.
Hakuna mshindi hata mmoja ambaye leo hii tunaweza kuanza kutaja orodha ya nyimbo alizofanya baada ya mashindano zilizohit kwenye radio na TV.
Washindi wengi ukianzia Jumanne Idd, Misoji Nkwabi hadi Pascal wameishia kutoka nyimbo ‘jojo’ zilizovinjari kwenye mawimbi ya radio kwa wiki ama miezi michache tu kabla hazijasahaulika kabisa na kutupwa kapuni.
Mbaya zaidi ni kuwa washindi wengi hushindwa kuuendeleza umaarufu walioupata kwa kuonekana kila wiki kwenye runinga na kujipatia mashabiki ambao huwapigia kura, na kujikuta wakianza upya tena kuwashawishi wapenzi wa muziki kuwa wanaweza kuhimili mkondo mkuu wa muziki (mainstream music).
Maswali ni mengi ya kujiuliza kuhusiana na ukweli huu. Kwanini mshindi aliyejipatia zawadi ya shilingi milioni 30 ama 40 anashindwa kupata mafanikio baada ya mashindano ilihali kipaji chake ndo kimempa ushindi?
Ama washindi wa BSS siku zote huwa ni wasanii wazuri katika kundi la wasanii wabovu. Mfano huo unatufanya tufananishe na mwanafunzi anayeonekana na akili nyingi katika darasa la ‘mbumbumbu’!
Ama wasanii wenye vipaji huchelea kujiandikisha kwenye mashindano hayo kutokana na utaratibu mbovu wa uchuchaji wa vipaji? Kwanini ni rahisi zaidi kwa msanii mwenye kipaji kufanikiwa akiamua kutoka kwa njia ya kawaida na sio kupitia BSS?
Ingawa uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya washindi wa mashindano ya aina hii hata yale makubwa duniani huishia kwenye shimo hilo sawa na wa BSS, baadhi ya washindi wa American Idol wamefanikiwa sana. Mfano mzuri ni pamoja na Kelly Clarkson, Ruben Studdard, Fantasia Barrino, Carrie Underwood na Jordin Sparks.
Mfumo wa kupata mshindi kwa njia ya kura za watazamaji mara nyingi huishia kumpata mshindi mbovu. Hii ni kwasababu watazamaji wengine huwapigia kura washiriki wanaovutia kwa sura, muonekano ama tabia na sio uwezo wa kuimba.
Mfano mzuri ni mashindano ya mwaka huu ya American Idol. Kila mtu anayeujua muziki alikuwa anajua mshindi atakuwa Joshua Ledet ama Jessica Sanchez. Kama ulikuwa mfuatiliaji mzuri wa American Idol 2012 iliyofikia tamati mwishoni mwa mwezi uliopita utakubali kuwa kati ya hao washiriki wawili mmoja wapo alitakiwa kuwa mshindi kutokana na kila mmoja kuwa na uwezo mkubwa kiuimbaji.
Lakini cha ajabu alishinda Phillip Phillips, kijana aliyekuwa kipenzi cha wasichana kutokana na kuwavutia kwa sura lakini mwenye uimbaji unaoweza kukufanya uzibe masikio kumsikiliza. Mfano huo unatuambia kuwa, upatikanaji wa mshindi kwa njia ya kura siku zote una matatizo kama hautachanganywa na njia zingine kwa asilimia sawa.
Ni ukweli kwamba washiriki waliokamata nafasi za chini kwenye Top 5 za BSS, ndio ambao walau wanafanya muziki wa kueleweka. Mfano mzuri ni Abubakar Mzuri, Baby Madaha na Peter Msechu ambaye baadaye alikuja kung’ara kwenye mashindano mengine makubwa zaidi ya Tusker Project Fame.
Pamoja na maandalizi hayo makubwa ya EpiqBSS, waandaaji wanatakiwa kuja na mkakati wa ziada kwanza kurudisha heshima yake iliyoshuka kwa kasi na pia kuja na njia za ubunifu kuhakikisha kuwa mshindi anaendelea kuwa nyota mwenye uwezo wa kuteka soko kuu la muziki wa Tanzania.
Pengine kuna haja waandaaji kufikiria njia mpya ya kumpata mshindi bila kutegemea kura za watazamaji ambazo hukaa kishabiki zaidi bila kuzingatia vipaji binafsi vya washiriki.
Marafiki 10 waliochaguliwa kuwanoa washindani wa mwaka huu wanatakiwa wachangie kwa walau asilimia hamsini kumchagua mshindi na hamsini zilizobaki zitokane na kura za watazamaji.
Itakuwa haina maana mshindi atakayepata kitita cha shilingi milioni 50 kuishia kutoa wimbo utakaochezwa kwa mwezi mmoja na kisha kushindwa kutoa nyimbo zingine nzuri.
Lasivyo watatufanya tuamini kuwa, pesa hizo hutolewa kwa mshindi ili azitumie katika biashara na muziki aufanye kama Plan B.
SOURCE