|

‘Lulu’ anawapa wakati mgumu askari magereza




Richard Bukos na Sifael Paul
IMEBAINIKA kuwa staa wa picha za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anawapa wakati mgumu askari magereza na polisi kufuatia ulinzi mzito wanaolazimika kumpatia wakati wa kumpeleka mahakamani na kumrejesha mahabusu kwenye Gereza la Segerea, Dar es Salaam, Amani linafunguka.
Baada ya wiki kadhaa mambo kutulia na ulinzi kuwa wa kawaida tofauti na siku ya kwanza alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jumatatu wiki hii hali hiyo ilijirudia ambapo Lulu ambaye anakabiliwa na kesi ya kifo cha Steven Kanumba alifikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akiwa na ulinzi wa kutisha.
Amani lilimshuhudia Lulu akishushwa mahakamani hapo akiwa mtuhumiwa pekee kwenye basi huku akisindikizwa na askari magereza wanawake zaidi ya kumi.
Mbali na askari magereza wanawake, kulikuwa na difenda la magereza lenye king’ora lililokuwa limejaa askari magereza wanaume na polisi wa kawaida.
ULINZI MAHAKAMANI
Mara baada ya ‘Kalulu Kadogo’ kufikishwa mahakamani hapo walipokezana na polisi wa mahakamani na katika kufumba na kufumbua, kila kona kulikuwa na askari waliokuwa wameimarisha ulinzi nje na ndani ya eneo hilo.
Maafande hao walishuhudiwa wakiwa wamevaa majaketi yasiyopenya risasi (bullet proof), kofia za chuma huku wakiwa na ‘mabunduki’ aina ya SMG zilizokuwa zimejaa risasi na mikanda ya risasi za ziada.
Wakati baadhi wakitanda ndani ya mahakama wakiwa wamemzunguka Lulu, wengine walizagaa nje huku wakizuia watu kukatizakatiza ovyo.
WAOMBA MAMBO YAISHE
Amani lilizungumza na baadhi ya askari hao wa kike ambao walionekana kutamani kesi hiyo iendeshwe haraka ili mambo yaishe kutokana na mshikemshike wanaokutana nao wakati wa kumpeleka Lulu mahakamani na kumrejesha gerezani.
Kuna baadhi waliokwenda mbali wakidai wanatamani hata kuhama vituo vyao vya kazi kutokana na mikikimikiki wanayokutana nayo wanapotakiwa kumpeleka Lulu mahakamani.
Ilidaiwa kuwa inapofika siku ya kumpeleka Lulu mahakamani, hulazimika kusitisha udhuru wowote kama kuwa wagonjwa hivyo kuzishangaza familia zao kwani wanapoulizwa kulikoni wanasema ni siku ya staa huyo na kila askari anakuwa ‘stendibai’.
Kwa muda wa saa mbili mahakamani hapo huku mawakili wakibishana juu ya umri wa Lulu, ratiba zote zilisitishwa kwani shughuli ilikuwa ni hiyo tu.
‘AMA KWELI ANAWATESA ASKARI’
“Ama kweli Lulu anawatesa hawa askari, kila mmoja yuko ‘bize’ na suala la ulinzi wake,” alisikika dada mmoja aliyefika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo.
KESI YAPIGWA KALENDA
Baada ya mawakili hao kushindwa kufikia muafaka wa umri kama ni miaka 17 au 18, kesi hiyo ilipigwa kalenda hadi Juni 11, mwaka huu ndipo utata wa umri wa Lulu utakapopatiwa ufumbuzi ili kuruhusu kesi hiyo ianze kusikilizwa.
TUMEFIKAJE HAPA?
Lulu ni mshukiwa wa kwanza katika kesi ya kifo cha aliyekuwa mpenzi wake na staa mkubwa wa filamu za Kibongo, Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake maeneo ya Sinza Vatican City, Dar.

Posted by Unknown on 1:40 PM. Filed under , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added