|

Vita kati ya imani ya Freemason na makanisa


SASA ni vita! Si vingine ni kati ya imani ya Freemason na makanisa. Mchungaji wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (E.A.G.T) lililopo Kipunguni B, Dar, Julius Mwamkamba amevujisha siri ya kushawishiwa na Freemason ajiunge nao kwa makubaliano ya kumjengea kanisa la kisasa, Risasi Jumamosi linatiririka nayo.
MCHEZO ULIVYOANZA
Akizungumza na mapaparazi wetu juzikati, jijini Dar, Mchungaji Mwamkamba alisema awali alitoa matangazo na pia kutuma ujumbe mfupi wa simu ‘SMS’ kwa watu mbalimbali akiomba mchango wa fedha ili aweze kujenga kanisa lake, lakini bila matarajio yake, namba zake ziliangukia mikononi mwa watu hao.
“Nilitarajia kupanua kanisa langu hivyo nilihitaji mchango wa fedha kwa ajili ya ujenzi, nikatoa tangazo kwa watu mbalimbali pamoja na kutuma SMS kwa marafiki zangu.
“Siku moja nilipigiwa simu na watu nisiowajua, wakaniambia wanataka kukutana na mimi ili wanisaidie fedha  za ujenzi wa kanisa langu.
“Nilikubali, nikaenda kukutana nao pale Ubungo. Walianza kunieleza jinsi walivyoamua kunisaidia kujenga hekalu la Mungu huku wakisema wananipa fedha za kutosha na kuagana na umaskini,” alisema Mchungaji Mwamkamba.
Aliendelea kudai kuwa watu hao walisema lengo lao ni kumpa kiasi chochote cha fedha ambacho kilikuwemo kwenye ‘brifkesi’ kwa ajili ya ujenzi huo.
“Waniliambia wananipa kiasi chochote cha fedha ninachokihitaji, lakini iwe siri yangu na wao, halafu wakasema waumini katika kanisa langu wataongezeka.

MCHUNGAJI AZIDI KUFICHUA
“Wakaniambia wamefanya hivyo kwa watumishi wengi wa Mungu hapa Tanzania ambao kwa macho ya kawaida huwatambuliki kama ni wafuasi wa Freemason na wanafanya ishara na miujiza mingi huku makanisa yao yakiwa na idadi kubwa ya waumini.”

APEWA MKATABA
Baada ya mazungumzo ya muda mrefu na kabla mchungaji huyo hajasema ndiyo au hapana, alipewa mkataba wenye maelekezo ya jinsi ya kujiunga ili aanze kula mema ya nchi na kuuaga umaskini kwa muda mfupi.
“Walinipa mkataba, una nembo ya Freemason, lakini wakaniambia ni lazima nibadili dini, nianze kuvaa nembo ya mwewe na nyoka na kumtoa kafara mke wangu au mwanangu nimpendaye kama sadaka ya shukrani kwa mungu wao,” alisema mchungaji.

AWACHOMOLEA WAZI
“Niliposikia masharti hayo, ghafla nilisikia uchungu moyoni, nikakataa, nilisimama haraka sana na kuondoka kwa mwendo wa haraka, kama nakimbia. Wakaanza kunizomea huku wakitoa ishara ya kuvunja vidole viwili ambayo ni moja ya alama za Freemason,” alisema mchungaji huyo.

KWA NINI NI VITA?
Hivi karibuni, Mchungaji wa Kanisa la Good News for All Nations, Mark Diganyeka alitoa alama za kuwatambua watumishi wa Mungu ambao ni waumini wa dini ya Freemason na kusema kuwa waumini wawe makini kuwabaini.
Miongoni mwa alama hizo alisema ni pamoja na kuvunja vidole kwa haraka wakati wakihubiri na kuvaa pete kubwa kwa ajili ya kufanyia miujiza wawapo madhabahuni.
Kwa tafsiri ya Mchungaji Diganyeka na hayo aliyokutana nayo Mchungaji Mwamkamba, ni dhahiri  makanisa yameingiliwa na Freemason hivyo kuanza kutimia kwa yale maneno kwamba, imani hiyo itawavaa watumishi wa Mungu kabla ya kurudi kwa Yesu Kristo.

Posted by Unknown on 9:41 PM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added