|

Wanne wajitokeza kumrithi Nchunga Yanga


WANACHAMA wanne wa klabu ya Yanga, wamejitokeza kuwania nafasi ya Uenyekitim katika siku ya mwisho ya zoezi la kuchukua na kurudisha fomu tayari kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam baadaye mwezi ujao, huku wanachama wengine wanne wakiwemo vigogo wawili serikalini wakijiondoa kwenye kinyang'anyiro.

Sambamba na nafasi hiyo ya Uenyekiti, wagombea wengine wanne wamejitokeza kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti. Mpaka jana jioni, wanachama 33 walikuwa wameomba kugombea.

Wanachama walioshindwa kurejesha fomu na hivyo moja kwa moja kujiondoa ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Elichimu Maswi, kigogo wa Tanesco Isack Chanji, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu na Muzamil Katunzi.

Walioomba nafasi ya mwenyekiti ni John Jambele, Edgar Chibura, Sarah Ramadhani na mfanyabiashara mmoja maarufu jijini Dar es Salaam.Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti ni Ayubu Nyenza, Clement Sanga, Stanley Kevela na mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayai ‘Tembele’ ambaye awali alichukua fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe kabla ya jana kubadili uamuzi.

Kwa upande wa wajumbe waliorudisha fomu ni Lameck Nyambaya, Ramadhani Kampira, Mohamed Mbaraka ‘Bin Krebu’, Ramadhan Said, Edgar Fongo, Ahmed Gao, Beda Tindwa, Musa Katabalo, Jumanne Mwamenywa, George Manyama, Gadeuncius Ishengoma, Haron Nyanda, Omary Ndula, Shaban Katwila, Justine Baruti, Abdallah Sharia, Jamal Kisongo, Peter Haule, Ally Mayai na Stanley Kevela ‘Yono’ ambao pia wanagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti

Akizungumza kwenye ukumbi wa mikutano wa Yanga jana mwakilishi wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Chabanga Dyamwale alisema alilaani makundi ndani ya klabu hiyo ambayo tayari yameanza kutoa maneno yenye kuhatarisha mlolongo mzima wa uchaguzi.

Dyamwale alisema kamati ya kuratibu zoezi la kuchukua na kurejesha fomu ndani ya klabu hiyo ikisimamiwa na Katibu wa Kamati ya Uchaguzi, Francis Kaswahili imehitimisha zoezi hilo vizuri muda wa 10 jioni jana.

Leo kamati hiyo chini ya John Mkwawa itapitia fomu za wagombea na kesho majina ya waliopitishwa yatawekwa wazi, wakati Juni 14 ni kipindi cha pingamizi hadi Juni 18, kabla ya usahili kufanyika Juni 19 na matokeo yakitangazwa siku hiyo hiyo.

Juni 24, Kamati itatoa fursa ya kukatwa rufaa kwa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mpaka Juni 26.

Juni 27-Julai Mosi, kamati ya TFF itakutana kusikiliza rufaa kama zitakuwepo na kutangaza matokeo ya rufaa hizo, ambapo Kamati ya Uchaguzi ya Yanga itatangaza rasmi majina ya wagombea waliopita.

Posted by Unknown on 11:26 PM. Filed under , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added