|

Simba Wafanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Urafiki


Simba SC wakishangilia pamoja na kombe lao baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Urafiki jana.
Na Wilbert Molandi
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba, jana walifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Urafiki baada ya kuifunga Azam kwa penalti 3-1, kufuatia dakika 90 za mchezo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Simba ndani ya dakika 90 yalifungwa na Felix Sunzu katika dakika ya 29 na Mwinyi Kazimoto aliyefunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 90, wakati yale ya Azam yalifungwa na Hamis Mcha (45) na John Bocco (81)
Katika mikwaju ya penalti, Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah na Kigi Makasi ndiyo walioifungia Simba wakati Haruna Moshi ‘Boban’ alikosa, wakati Azam ikipata penalti yake kupitia kwa Mcha huku Haji Nuhu, Himid Mao na Ibrahim Mwaipopo wakikosa.
Wakati ikionekana kuwa Simba wangekwenda mapumziko wakiwa wanaongoza, Azam walifanya shambulizi la kushtukiza na kufanikiwa kupata bao katika dakika ya 45 baada ya Tchetche kumpigia krosi Hamis Mcha aliyeifungia Azam bao la kusawazisha.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mashambulizi ya kushtukiza lakini ni Azam ndiyo iliyotangulia kujipatia bao lakini Simba wakasawazisha.
Mara baada ya mchezo huo Kocha wa yanga Tom Saintfiet ambaye alishuhudia mchezo huo uwanjani hapo akiwa jukwaani kwa mashabiki wa Yanga alisema Simna ni timu nzuri na imecheza vizuri, pia alimsifia Sunzu kwa kusema kuwa anatakiwa kuchungwa kwa kuwa anaonyesha ana madhara makubwa.
Kocha wa Simba, Milovan Circovic alisema hajaridhishwa na uimara wa wachezaji wake licha ya kuibuka na ushindi huo, hali ambayo inaleta hofu katika ushiriki wao wa michuano ya Kagame inayoanza kesho. Wachezaji ambao anadai hawakuwa imara ni Boban, Kazimoto na Juma Nyosso.
Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongala alilalamikia bao la pili la Simba kwa kudai kuwa mshambuliaji Danny Mrwanda alijiangusha eneo la hatari, hivyo hawakustahili kupata penalti iliyozaa bao la kusawazisha kwa wapinzani wao.

Posted by Bongo Flavor on 9:50 PM. Filed under , , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

Blog Archive

Labels

Recently Commented

Recently Added